Watu wanne walifariki na wanane bado wamelazwa hospitalini kufuatia kisa kinachoshukiwa kuwa na sumu kwenye chakula katika kaunti ndogo ya Kuria Magharibi, kaunti ya Migori.

Picha ya mkanda wa eneo la uhalifu. Picha: Getty Images.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ndogo ya Kuria Magharibi Bw.Cleti Kimaiyo alisema polisi walipokea ripoti kutoka kwa wananchi kwamba baadhi ya watu kutoka vijiji vya Kubweye na Kunguku wamelazwa katika kituo cha matibabu cha Samjomen kufuatia tukio linaloshukiwa kuwepo kwa sumu kwenye chakula.
Kimaiyo alisema askari hao kutoka kituo cha polisi cha Isebania walitembelea kituo hicho eneo la Mabera na kuthibitisha kuwa watu wanne ambao ni David Marwa mwenye umri wa miaka 52, Nyasenso Hisingo mwenye umri wa miaka 55, Mwita Manaigwa mwenye umri wa miaka 45 na Samson Moti mwenye umri wa miaka 52 walifariki dunia.
Alieleza kuwa watu wanane waliokunywa vyakula hivyo na vileo haramu pia walitibiwa katika kituo cha afya cha Samjomen kabla ya kuhamishiwa hospitali ya Migori level four kwa matibabu zaidi, na kuongeza kuwa hali zao bado zinaendelea kufuatiliwa.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo alisema ripoti kutoka hospitali ya Samjomen inaonyesha kuwa wagonjwa hao walikuwa na matatizo ya kupumua, kutapika, kuhara, na maumivu ya tumbo walipofikishwa katika kituo hicho.
Bw.Kimaiyo alisema miili ya wanne walioaga imepelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Akidiva ikisubiri uchunguzi wa maiti na polisi.
Alisema polisi walitembelea nyumbani kwa mmoja wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Nyasenso Hisingo katika kijiji cha Kubweye ambako inadaiwa wahanga hao walikula na kunywa.