Mganga wa kienyeji na mteja wake, mwanamke mwenye umri wa miaka 59, wote wamefariki baada ya kunywa mchanganyiko wa mimea yenye sumu.
Kwa mujibu wa taarifa, mkasa ulianza wakati mwanamke aliyeitwa Edith Chilanda alimwendea mtaalamu wa tiba za asili Kapoya Chiyesu kwa msaada kutokana na mguu wake kuvimba.
Kama ilivyo kawaida, Chiyesu alimpa mwanamke huyo dawa za mimea ambaye baadaye alianza kutapika na akapelekwa hospitalini haraka.
Wananchi walimkabili mganga huyo wa jadi na kumtuhumu kwa kumpa mteja dawa za sumu.
Kulingana na afisa mkuu wa mkoa wa Kaskazini-Magharibi, Dennis Moola, familia na wakazi wenye ghadhabu walimpeleka mganga huyo kwa polisi wa Kabompo.
Walipokuwa bado kituoni, familia ilipokea taarifa kuwa jamaa yao alikuwa amefariki kabla ya kupata matibabu.
Kwa lengo la kuthibitisha kuwa dawa hiyo haikuwa na madhara, Chiyesu pia alikunywa mchanganyiko huo baada ya hapo naye akaanza kutapika.
Mganga huyo wa jadi alipelekwa hospitali ya Wilaya ya Kabompo lakini pia alitangazwa kufariki alipofika.
Afisa alifichua kuwa polisi walitembelea nyumba ya mwanamke aliyefariki na kukusanya mizizi katika mfuko wa ukwa pamoja na mimea iliyokatwa kwenye sufuria ambayo inasadikiwa kuwa waliyotumia marehemu wote.