Watu kadhaa Wahofiwa Kufariki Kwenye Ajali ya Basi la Shule eneo la Kendu-Homa Bay.

Watu kadhaa wahofiwa kufariki baada ya ajali mbaya kutokea kwenye makutano ya Pala-Homa Hills kwenye barabara kuu ya Kendu-Homa Bay mnamo Ijumaa, Mei 5.

Picha ya basi lililopata ajali 5.5.2023

Basi la shule liliripotiwa kubingiria na kujeruhi watu kadhaa huku wengine wakihofiwa kufariki.

Wakaazi wa eneo hilo walikimbia kusaidia kuwaokoa waathiriwa huku wafanyikazi wa dharura walifika baadaye kuwasafirisha hadi hospitali za karibu kwa usimamizi wa huduma ya kwanza.

Basi la Shule ya Sekondari ya ACK GUU liliripotiwa kuwa na watu 39.

Kwa mujibu wa walioshuhudia ajali hiyo, basi hilo lilipinduka wakati likijaribu kukwepa kugongana uso kwa uso na lori.

Watu waliojionea pia waliripoti kuwa baadhi ya waathiriwa walikuwa wakisafiri kwenda kwenye mazishi.

Kutokana na picha hizo zilizosambazwa kwa wingi, basi la shule liliharibiwa vibaya sehemu za mbele na sehemu nyingine za gari, ikiwa ni pamoja na kupasuliwa vioo.

Kulingana na kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Rachuonyo Kaskazini Lydia Parteyie, basi hilo lilitoka nje ya barabara kabla ya kuanguka kwenye mtaro uliokuwa karibu.

Aliongeza kuwa shughuli ya uokoaji inaendelea ili kubaini waliopoteza maisha.

Leave a Reply