Waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida, anusurika kifo katika mlipuko wa bomu akihutubia umma

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida alinusurika kifo Jumamosi baada ya bomu linaloonekana na kufuatiwa na mlipuko mkubwa na moshi mweupe unaopanda kwenye ukumbi ambapo alikuwa karibu kuanza hotuba katika jiji la Wakayama, jarida la The Japan Times limeripoti.

Picha kutoka eneo la tukio. Hisani

Wachunguzi walikamata vitu viwili vya silinda kutoka eneo la tukio vinavyoaminika kuwa vilipuzi, NHK iliripoti.

Kilipuzi kimoja kililipuka wakati wa tukio, wakati kiingine kikikamatwa na afisa wa polisi wakati mshukiwa, Ryuji Kimura, mwenye umri wa miaka 24 kutoka Kawanishi, Mkoa wa Hyogo, akizuiliwa, jarida hilo liliripoti.

Mshukiwa huyo hadi sasa hajajibu maswali ya polisi lakini amesema atazungumza mara wakili wake atakapowasili.

Hakuna majeruhi walioripotiwa kufuatia tukio hilo.

Kanda za video zilionyesha watu katika Bandari ya Uvuvi ya Saikazaki huko Wakayama wakikimbia kutafuta hifadhi mwendo wa 11:25 a.m., huku mwanamume huyo akilemewa kwanza na wavuvi wawili wa eneo hilo.

Wengine kadhaa na maafisa wa polisi katika eneo la tukio wakamshikilia mshukiwa chini. Chapisho la Twitter pia lilionyesha kuwa watu walikuwa wakitoroka kutoka eneo la tukio.

Kishida ambaye alikuwa akitembelea bandari hiyo kwa ajili ya kutoa hotuba ya kumuunga mkono mgombea wa chama cha Liberal Democratic katika uchaguzi mdogo utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu, aliondoka eneo la tukio bila kujeruhiwa baada ya tukio hilo lililotokea alipokuwa akizungumza na mgombea wa chama chake tawala cha Liberal Democratic Party.

Tukio hilo linakuja miezi tisa tu baada ya kuuawa kwa Waziri Mkuu wa zamani Shinzo Abe kwa bunduki ya kujitengenezea nyumbani alipokuwa akiendesha kampeni za LDP katika Jimbo la Nara, ambalo linapakana na Wakayama.

Kuuawa kwa Abe kulisababisha polisi kurekebisha sheria za ulinzi wa VIP.

 

Leave a Reply