Mzee wa miaka 60 huko Mwea, Kaunti ya Kirinyaga, nchini Kenya amejitoa uhai baada ya kudaiwa kugundua mkewe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine wa miaka 24.
Mwili wake ulipatikana umening’inia kwenye paa la nyumba yao huku akiwa amefungwa kamba shingoni.
Henry Kariuki, Chifu wa Kijiji cha Kiarukungu, alifichua kuwa marehemu alizuru afisi yake siku ya Jumatano akielezea kutamaushwa kuhusu uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa yao.
Baadaye chifu huyo alifahamishwa kuhusu kisa ambapo mwanamume mmoja alimvamia mkewe kwa panga, ndipo akagundua kuwa ni marehemu ndiye aliyefanya kitendo hicho.
Mke aliripotiwa kutibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini. Hata alitangulia kuandikisha ripoti katika Kituo cha Polisi cha Wang’uru.
Chifu Kariuki alisema kuwa mwanaume huyo aliazimia kumuacha mkewe.
Ripoti zinaonyesha kuwa mwanamke huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni mchuuzi wa nyanya kijijini hapo.
“Hatukufikiri kwamba mambo yangeisha hivi kwa sababu alikuwa amesema ameamua kuwaacha wawili hao wafanye walivyotaka,” chifu huyo aliongeza.
Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Mwea Mashariki Daniel Kitavi alithibitisha kisa hicho, akisema marehemu alitakiwa kufika kituoni kurekodi taarifa ila akapatikana amefariki.