Afisa wa Polisi Amuua Afisa Mwenzake Kwa Kumfyatulia Risasi Migori.

Afisa wa polisi alikamatwa Jumapili dakika chache baada ya kumpiga risasi na kumuua mwenzake katika maeneo ya Awendo, kwenye kaunti ya Migori.

Inadaiwa alimuua anayefanya kazi nae katika eneo la kuhifadhia silaha la Kitengo cha Ulinzi wa Miundombinu muhimu katika kituo cha polisi cha Awendo.

Polisi walisema mshukiwa alidaiwa kumuua mwenzake Elijah Anyira kwa kumpiga risasi kutumia bunduki aina ya AK-47 mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi mnamo Februari 19, 2023.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Suna Mashariki, Hesau Ochorokodi alisema mshukiwa alikuwa akirudisha bunduki yake kwenye ghala baada ya kazi ya usiku alipomfyatulia risasi mwenzake.

Afisa aliyefyatuliwa risasi alikimbizwa katika hospitali ya Rapcom kwa matibabu lakini alitangazwa kuwa amefariki alipofika.

Bosi huyo wa polisi alisema sababu ya mauaji hayo haijafahamika, ila wamesikia mshambuliaji alipanga kujitoa uhai kwa sababu zisizojulikana.Hivyo uchunguzi zaidi unaendelea

Baada ya kupiga risasi, aliiacha silaha yake kituoni na kuelekea nyumbani kwake ambapo alikamatwa dakika chache baadaye.

Bunduki yenye risasi 27 iliyotumika katika mauaji hayo ilipatikana katika eneo la tukio.

Kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na hali kama hii na nyinhine kama vile kujitoa uhai, mamlaka za polisi zimezindua huduma za ushauri nasaha. Tume ya Kitaifa ya Huduma kwa Polisi imeanzisha kitengo maalumu ili kushughulikia hali yao ngumu.

Leave a Reply