Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu Atangaza Matokeo ya KCPE 2022 Na Kuweka Wazi kuhusu KPSEA 2022.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu mnamo Jumatano, Desemba 21, alitoa matokeo ya Mtihani wa darasa la nane 2022 (KCPE).

Akizungumza katika ukumbi wa Mtihani House, Machogu alitangaza kuwa zaidi ya wanafunzi Milioni 1.2 walifanya mitihani ya kitaifa iliyoanza Novemba 18 huku mwanafunzi bora akipata alama 431.

Machogu alitoa matokeo hayo muda mfupi baada ya kuyawasilisha kwa Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

“Watahiniwa wote ambao ninatoa matokeo yao leo watadahiliwa kidato cha kwanza chini ya sera ya mpito ya asilimia 100,” alisema.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu mnamo Jumatano, Desemba 21 akitangaza matokeo Picha:Wizara ya Elimu Kenya twitter

Kiingereza na Kiswahili viliandikisha matokeo bora zaidi ikilinganishwa na matokeo ya KCSE ya 2021.

Wanafunzi 9443 walipata zaidi ya alama 400. Waliopata alama kati ya 300 na 399 walikuwa wanafunzi 307,756 , waliopata kati ya 200 hadi 299 ni wanafunzi 699,593, waliopata 100 na 199 walikuwa 1270  huku waliopata alama kati ya 1 na 99 wakiwa 6.

Watahiniwa waliofanya mitihani yao katika hospitali mbalimbali  walikuwa  147.

Pia ilibainika kuwa watahiniwa waliochini ya miaka 12 walikuwa 31,494.

Katika Matokeo hayo ya KCPE 2022, Lewis Otieno Omondi na Fwaro Makokha Robinson waliibuka wa baada ya kila mmoja kupata daraja A katika masomo yote matano yaliyotahiniwa na Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC) jumla ya alama 431 kati ya alama 500.

Lewis alisomea Shule ya Msingi ya Wavulana ya St. Peters Mumias katika Kaunti ya Kakamega, kama ilivyothibitishwa na walimu wake.

Fwaro, kwa upande mwingine, alikuwa mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Christ the King huko Bungoma.

Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC) pia lilitangaza kuwa matokeo ya mitihani ya kitaifa ya Darasa la Sita yatatolewa Januari 16, 2023 kupitia kwenye tovuti ya shule zao.

“Wanafunzi watapata ripoti za kibinafsi na zote hizi zitapakiwa kwenye tovuti ya shule mnamo Januari 16, 2023,” Mkurugenzi Mtendaji wa KNEC David Njeng’ere alisema.

Matokeo hayo hayatatumika kuweka watahiniwa katika shule za sekondari za awali bali kuangalia maendeleo ya wanafunzi.

Mkuu huyo wa KNEC aliongeza kuwa baraza la mitihani litatoa ripoti tatu kuhusu KPSEA: mtu binafsi, shule mahususi na ngazi ya kitaifa.

“Ripoti ya kitaifa itatoa mrejesho kwa wadau wa elimu kuhusu maeneo ambayo yanahitaji uingiliaji kati, itaonyesha uwiano wa wanafunzi katika kila ngazi ya ufaulu kwa somo ambapo tunahitaji kufanya afua.

“Kila shule itapokea ripoti mahususi zitakazoainisha maeneo ambayo wanafunzi walikuwa na changamoto ili waendelee na safari ya uboreshaji,” alifafanua.

Mkurugenzi Mtendaji wa KNEC alishikilia kuwa watahiniwa hao watahifadhiwa katika shule zao za msingi kwa elimu yao ya upili.

Wanafunzi 1,287,597 wa Darasa la Sita walisajiliwa kwa mitihani ya kitaifa ya KPSEA 2022.

Leave a Reply