Tshala Muana Mwanamziki Mkongwe Aaga Dunia

 

Msanii mkongwe wa miziki aina ya Rhumba kutoka taifa la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Tshala Muana ameaga dunia.

Taarifa hizo za tanzia kutoka taifa hilo zilisambazwa kote duniani Usiku wa kuamkia Jumamosi ambapo wapenzi wa Rhumba walijumuika mitandaoni kutuma risala za rambi rambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa mama huyo mkongwe.

Picha ya Marehemu Msanii Tshala Muana

Mtangazaji mkongwe nchini Kenya ambaye ni mpenzi wa miziki ya Rhumba, Fred Obachi Machokaa alidhibitisha habari hizi kupitia video fupi aliyoipachika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

“Habari za kuvunja moyo kutoka DRC.

”Habari za kuvunja moyo kutoka DRC. Malkia wa Mutwashi Tshala Muana anayejulikana pia kama Elizabeth Muidikay amefariki dunia asubuhi ya leo kutokana na matatizo ya Shinikizo la Damu.
Kwa niaba ya #RogaRoga na mashabiki wote wa Rhumba nchini Kenya tunatuma rambirambi zetu za dhati.,” Machokaa alisema kwa majonzi.

Tshala Muana alizaliwa mwaka wa 1958 nchini Kongo kama Elizabeth Muidikay. Alianza kazi yake ya kisanii kama mcheza densi wa bendi ya muziki ya Tsheke Tsheke Love mwaka 1977 kabla ya kugeukia kuimba. Anajulikana kwa nyimbo kadhaa kama vile Vuluka Dilolo, Karibu Yangu, Chena, Nasi Nabali,  na nyingine nyingi ambazo zilimwezesha kushinda tuzo nyingi kitaifa na kulipalilia jina lake kama mwanamuziki wa Rhumba wa Kike kutoka taifa hilo.

Mwaka 1964, wakati Muana Muidikay alipokuwa na umri wa miaka 6, baba yake aliuawa wakati wa mgogoro wa Kongo. Alilelewa na mama yake, ambaye alikufa mnamo 2005. Hajawahi kuolewa, mwandamani wake wa karibu muda wote amekuwa ni mtayarishaji wake, Claude Mashala, mwanasiasa ambaye waliachana baada ya kupata mtoto mmoja wa kike.

Mnamo Novemba 2020, Muana alikamatwa na Shirika la Kitaifa la Ujasusi nchini Kongo kwa kutoa wimbo ‘ Igratitude’ uliokisiwa kukejeli uongozi wa rais Felix Tshishekede.Uliosambazwa sana mitandaoni na njia pekee ya kuuzima ilikuwa kumkamata na  kushrutisha wimbo huo uondolewa katika majukwaa yote ya kupakua miziki.

Mpaka kifo chake, Tshala Muana alikuwa mwenye umri wa miaka 64 na amemuacha mtoto mmoja wa kike.

Leave a Reply