Mmoja wa washukiwa waliotengeneza bomu lililolipua ndege angani amekamatwa.

Mwanamume mmoja raia wa Libya anayetuhumiwa kutengeneza bomu lililoharibu ndege ya Shirika la Pan Am Disemba 21, 1988, amekamatwa nchini Marekani.

Picha ya Mabaki ya ndege Boeing 747 Picha hisani: Reuters

Ndege hiyo, Boeing 747, ilikuwa ikielekea New York kutoka London  ililipuka ikiwa angani juu ya mji mdogo wa Lockerbie, Scotland, na kuwaua Watu 259 waliokuwemo ndani ya ndege na wengine 11 wakiuawa wakati mabaki yalipoharibu nyumba zao 

Waendesha mashtaka wa Scotland wamesema Familia za wale waliouawa kwenye mkasa huo zimefahamishwa kwamba Abu Agila Muhammad Masud sasa yuko kizuizini.

Awali alikuwa anashikiliwa nchini Libya akishukiwa kushiriki kwenye mashambulizi dhidi ya klabu moja ya usiku mjini Berlin mwaka 1986.

Aidha,Marekani ilitangaza mashtaka dhidi ya Abu Agila Masud miaka miwili iliyopita, kwa madai kuwa alikuwa na jukumu muhimu katika shambulio la bomu la tarehe 21 Disemba, 1988.

Hata hivyo,Wizara ya Sheria ya Marekani imethibitisha kumshikilia Mshukiwa huyo, ikisema kuwa anatazamiwa kufikishwa Mahakamani hivi karibuni mjini Washington, DC.

Masud ni Afisa wa tatu wa ujasusi wa Libya kufikishwa Mahakamani nchini Marekani kwa mashambulizi dhidi ya ndege hiyo ya shirika la Pan Am iliyokuwa ikiruka kutoka London kwenda New York. 

Leave a Reply