Waziri wa elimu nchini Kenya,Ezekiel Machogu ameweka wazi kuwa matokeo ya mitihani ya darasa la nane KCPE iliyokamilika mwanzoni mwa mwezi wa Desemba yatatangazwa wiki kesho.

Machogu alisema kuwa wizara yake imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa hakuna visa vya wizi wa mitihani ya kitaifa ya sekondari KCSE ambayo inaendela kote nchini.
Machogu alikuwa akiyazungumza haya wakati wa hafla moja ya mazishi eneo bunge la Nyaribari Masaba ambapo alikuwa mbunge kabla ya kuwania ugavana wa kaunti ya Kisii katika uchaguzi uliopita wa Agosti 9.
“ Wiki ijayo tunatangaza matokeo ya mtihani wa KCPE na hutasikiliza kesi zozote za udanganyifu chini ya uongozi wa Machogu. Upangaji wa alama za Cheti cha Elimu ya Sekondari cha Kenya (KCSE) unaendelea vyema na ninakuhakikishia, matokeo hayatakuwa na dosari zozote ,” alisema waziri Machogu.
Matokeo hayo yatatoka siku chache tu kuelekea sherehe za Krismasi, wakati ambapo mitihani ya kidato cha nne itakuwa inakamilika pia kote nchini.
KCSE iling’oa nanga mwanzoni mwa mwezi hu wa Desemba kwa wiki tatu hadi tarehe 23 Desemba.
Haya yatakuwa matokeo ya kwanza kutangazwa na waziri huyo mpya ambaye aliteuliwa na kupitishwa na bunge kuhudumu katika baraza la mawaziri wa Rais Ruto kama waziri wa elimu, wizara ambayo ilikuwa imeshikiliwa kwa muda mrefu na waziri profesa George Magoha.