Polisi wamemkamata mwanamume mwenye umri wa miaka 30 anayesemekana kuwa ndiye mpangaji mkuu wa shambulio baya la maiti na gari la kubebea maiti la Yatta Funeral Home iliyoko Machakos .
Akithibitisha kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Yatta Bernard Rono anasema kuwa mshukiwa ni mtoto wa mmiliki wa ardhi hiyo ambapo chumba cha kuhifadhia maiti kimejengwa.
Novemba 28 asubuhi, wakaazi waliamka na kusikia habari za kushtua kwamba genge lilikuwa limevamia chumba cha kuhifadhia maiti, na kuwachoma maiti kwa silaha zenye nchi kali kabla ya kuharibu gari la maiti katika kituo hicho.

Baada ya kisa hicho, mmiliki wa chumba cha kuhifadhia maiti Gideon Mule aliambia wanahabari kuwa mmiliki wa shamba hilo pamoja na familia yake walikuwa wameajiri wahuni ambao walihusika na kitendo hicho.
Mule anasema mwenye nyumba anamtaka aondoke bila kumlipa KSh7 milioni kama mahakama ilivyoagiza.”Anataka niondoke lakini mahakama ilikuwa wazi anilipe KSh7 milioni ili nihame. Sasa ameona mahakama ziko dhidi yake ameripoti vitisho na mashambulizi.
“Vioo vya magari ya kubebea maiti vimevunjwa hakuna hata kimoja kinachoweza kutumika hadi kitengenezwe. Mwili mmoja uliharibiwa kabisa hata familia iko hapa ina wasiwasi,” aliongeza.
Mule zaidi anasema Jumapili Novemba 27, mwenye shamba alikuwa ametishia kumuua.