Afisa wa Polisi Katika Kituo Cha Polisi awaua Wenzake kwa Bunduki.

Afisa mmoja wa polisi katika kituo cha polisi cha Moyale katika kaunti ya Marsabit nchini Kenya awaua wenzake wawili na kuwaumiza wengine wawili kabla ya kujiua.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, Konstebo Lawrence Kumber alifika kazini na kumkuta mwenzake Noah Odero kisha kumpiga kichwani kwa jiwe kubwa.

Kisha afisa huyo alichukua silaha na kuelekea katika eneo la kuhifadhi silaha kituoni humo.

Baadaye alikutana na maafisa wengine ambao walikuwa wameripoti kazini na kuwaua kwa kuwapiga risasi wawili huku mmoja akipata majeraha mabaya..

Wawili hao Ezekiel Matete na Francis Kokwe walifariki papo hapo huku Konstebo Abass Mohammed akipata majeraha ya risasi kwenye bega lake la kushoto.

“Afisa huyo aliyejeruhiwa alikimbizwa katika hospitalini ya Alhilal mjini Moyale na yuko katika hali mbaya,” taarifa hiyo inasema.

Baada ya kutekeleza unyama huo, Kumber alielekea katika nyumba yake na kujiua kwa kujipiga risasi kwenye kidevu.

Miili ya maafisa waliofariki imepelekwa katika makafani ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Moyale.

Kwa sasa kiini cha mauaji hayo hakijulikani lakini ripoti za awali zimedai kuwa visa kama hivyo katika idara ya polisi vinatokana na msongo wa mawazo kazini.

Leave a Reply