Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya ,IEBC ,Wafula Chebukati amemtangaza William Samoei Arap Ruto kuwa Rais wa tano wa nchi ya Kenya.Kufuatia uchaguzi uliofanyika Agosti 9,2022.

Ni Kinyang’anyiro kilichokuwa na Wagombea wanne akiwemo George Wajackoyah wa chama cha Roots aliyeshika nafasi ya tatu,Waihiga Mwaure wa chama cha Agano nafasi ya nne na mshindani mkuu wa Ruto Bwana Raila Omolo Odinga wa Muungano wa Azimio la Umoja.
Ruto alipata kura 7,176,141 ikiwa ni asilimia 50.49 ya kura za mwisho, huku Raila akipata kura 6,942,930 ikiwa ni asilimia 48.85.
Matokeo hayo yalitangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati katika kituo cha kitaifa cha kuhesabu kura cha Bomas of Kenya mnamo Jumatatu.
Ruto mwenye umri wa miaka 55 ni mwanasiasa wa Kenya aliyegombea urais wa UDA ndani ya muungano wa Kenya Kwanza katika uchaguzi wa urais wa 2022 . Katika uchaguzi wa urais wa 2013, Ruto alichaguliwa kuwa Naibu Rais pamoja na Rais Uhuru Kenyatta chini ya tikiti ya Muungano wa Jubilee.Amehudumu kama Naibu wa Rais kutoka 2013 mpaka sasa.
Pia amewahi kuhudumu kama Kaimu Rais wa Kenya (2014–2014),Waziri wa Kilimo wa Kenya kati ya mwaka 2008 na 2010.
Hata hivyo dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa IEBC kutangaza matokeo hayo,Makamishna wa IEBC 4 kati ya 7 wamejitenga na matokeo ya Uchaguzi huo wa urais huku wakihutubia Wanahabari kutoka Hoteli ya Serena jijini Nairobi.
Makamishna hao Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irene Masit wamekimbia Bomas na kuelekea katika Hoteli ya Serena ambako wamehutubia vyombo vya habari na kuyakana matokeo ya uchaguzi mkuu wa urais licha ya kuwa tume ilikuwa mshindi wa Urais.