Maafisa watatu wa usalama nchini Kenya wanaohusishwa na mgombea wa Ugavana wa Kisii, Manson Nyamweya waliaga dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana na pikipiki.

Akithibitisha ajali hiyo, Mbunge huyo wa zamani,Manson Nyamweya alisema kuwa watatu hao walihusika katika ajali ya barabarani eneo la Nyambunwa wakati mwanasiasa huyo akitoka kumzika mamake.
Kiongozi huyo wa chama cha Kenya National Congress (KNC) alisema kuwa dereva wa gari hilo alishindwa kulidhibiti baada ya kujaribu kukwepa kumgonga mtu na kukutana ana kwa ana na pikipiki iliyokuwa mbele.
Gari hilo lilibingiria mara kadhaa na kuwaacha watatu hao wakiwa wamefariki dunia na wengine wawili wakiwa na majeraha mabaya. Waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii ambapo wanapata matibabu.
“Ni kwa huzuni kubwa kwamba nathibitisha tumewapoteza maafisa wangu watatu wa usalama katika ajali mbaya ya barabarani eneo la Nyambunwa karibu na Shule ya Sekondari ya Nyamesocho. Gari walilokuwa wakisafiria lilikuwa likikwepa kumgonga mtu aliyekuwa akivuka barabara na kwa bahati mbaya likapoteza mwelekeo na kugongana na pikipiki. Lilibingiria mara kadhaa na katika hali hiyo watatu hao walifariki dunia,” alisema Mbunge huyo wa zamani wa Mugitango Kusini.
Pia alituma risala zake za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha yao. “Salamu zangu za rambirambi kwa familia na marafiki wa marehemu Nitahakikisha wanazikwa kwa heshima na pia ninatoa msaada wangu kamili kwa wafiwa. Nasimama kidete nao,” Mbunge huyo wa zamani alisema.
Watatu hao walioangamia ni Joel Ositu,Seth Omambia na Stephen Makori.