Wananchi wa Sudan wameendelea kuandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum na katika miji mingine ya nchi hiyo dhidi ya serikali ya kijeshi.
Kumekuwa na maandamano na machafuko makubwa Sudan katika miezi ya karibuni kufuatia jeshi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Wafanya maandamano wanataka wanajeshi waondoke madarakani, uongozi wa nchi ukabidhiwe raia, uchaguzi wa kidemokrasia uitishwe nchini humo sambamba na kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi nchini.
Haya yanajiri miaka miwili baada ya serikali iliyokuwa ikiongozwa na Omar Hassan al-Bashir kupinduliwa na serikali ya mpito kuanzishwa.
Baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa maelfu ya wananchi wa Sudan waliandamana usiku katika mitaa ya mji mkuu Khartoum na pia mbele ya jengo la bunge la taifa katika mji wa Umdurman magharibi mwa Khartoum. Askari usalama walifika mbele ya bunge na kuanza kuwanyunyizia gesi ya kutoa machozi na kufyatulia risasi ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika hapo ambapo mtu mmoja ameripotiwa kuuawa katika ghasia hizo.
Umoja wa Mataifa umeeleza kutiwa wasiwasi na kuongezeka kwa ghasia na uwezekano wa kutokea maafa ya binadamu na njaa nchini humo.