Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi imetangaza kuathirika kwa trafiki katika barabara nne kuu jijini Nairobi, mnamo Ijumaa Aprili 29. Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Msemaji wa polisi Bruno Shioso,siku ya Alhamisi Aprili 28.

Barabara hizo zitafungwa kufuatia Misa ya Wafu ya kitaifa ya rais mstaafu hayati Mwai Kibaki, itakayoandaliwa katika uga wa Nyayo.
Barabara ya Aerodrome na sehemu ya barabara kuu ya Uhuru kuanzia kesho saa moja asubuhi, zitaathirika na trafiki. Waendeshaji magari wanaotumia barabara ya Waiyaki kuelekea barabara kuu ya Mombasa watalazimika kugeukia kwenye mzunguko wa jumba la Nyayo, na kutumia barabara ya Kenyatta Avenue kuelekea Moi Avenue, na kisha mzunguko wa barabara ya Heile-Sellasie.
Waendeshaji magari pia wanaweza kuelekea uga wa City na kujiunga na barabara kuu ya Mombasa. Madereva wanaotumia barabara kuu ya Mombasa na wangependa kuingia katikati mwa jiji la Nairobi au kuelekea eneo la Westlands, watatumia barabara ya pembezoni mwa Southern Bypass.
Pia wanaweza kutumia barabara za Likoni, Enterprise na Lusaka kujiepusha na msongamano kwenye barabara kuu ya Uhuru.
Wananchi wanaotaka kuhudhuria misa ya kitaifa ugani Nyayo, wanatakiwa kuyaacha magari yao nje ya maegesho ya uwanja, kwa sharti kwamba magari yao yawe na vibandiko spesheli.
Vilevile Katibu msaidizi katika afisi ya Rais Kennedy Karanja, ambaye anaongoza maandalizi ya mazishi ya hayati Rais mstaafu Mwai Kibaki, amesema kwa sasa watu 15,000 pekee watahudhuria mazishi hayo eneo la Othaya na huenda serikali ikaongeza nafasi zaidi, iwapo idadi ya wageni itaongezeka.
Hayati Kibaki anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake katika kaunti ya Nyeri, siku ya Jumamosi Aprili 30.
Karanja alidokeza kwamba mwili wa hayati Kibaki utasafirishwa kwa barabara kutoka makavazi ya Lee, hadi nyumbani kwake Othaya.
Kulingana na katibu huyo msaidizi, wanajeshi wamechukua usukani na matayarisho ya misa katika uwanja wa Shule ya Othaya Approved na katika sehemu atakakozikwa yanaendelea.
Mwili wa hayati Kibaki umekuwa katika majengo ya Bunge kwa siku tatu, kutoa fursa kwa wananchi kuutazama na kutoa heshima zao za mwisho. Misa ya wafu itafanyika siku ya Ijumaa Aprili 29.
Asante kwa taarifa, hii ni muhimu Kwa ajili ya kujipanga kesho.