Watatu wauawa na wavamizi nje ya lango la shule huko Kerio Valley

Watu watatu wameuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Kerio Valley katika Kaunti za Pokot Magharibi,Kenya.

Watatu hao, wanawake wawili na mwanamume mmoja walikuwa wakielekea kufariji familia ambayo ilikuwa imepoteza jamaa yao walipovamiwa na kuuawa na wavamizi hao nje ya lango la shule ya msingi.

Wanawake hao wawili wenye umri wa kati ya miaka 40 wanasemekana kufa papo hapo huku mwanamume huyo akifariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Endo.

Wakizungumza na kituo imoja cha habari nchini humu wenyeji wa eneo hilo wamesema kwamba watu wanaoshukiwa kuwa majambazi takriban 15 walikuwa wamejificha kwenye kichaka kilicho karibu kabla ya kuwafyatulia risasi waathiriwa nje kidogo ya Shule ya Msingi ya Liter.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Marakwet Mashariki Simon Osumba alithibitisha vifo hivyo na kuongeza kuwa watu wanaoshukiwa kuwa majambazi walivamia shule ya Sekondari ya Lukuget saa tano asubuhi siku ya Ijumaa na kujaribu kuiba mifugo, lakini shambulio hilo lilizimwa.

“Tulikuwa bado tunatuliza mvutano katika Shule ya Sekondari ya Lukuget tulipopata taarifa kuwa shambulio lingine lilitokea Kaben. Tunaweza kuthibitisha kuwa watu watatu wamekufa. Tunajaribu kurejesha utulivu,” Osumba alisema.

Kufikia sasa mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi katika bonde hilo siku ya Jumatano na mwingine Alhamisi, na kufanya idadi ya waliofariki katika kipindi cha miezi saba iliyopita kufikia 70.

Kufuatia hali ya usalama kuzidi kudhorora huku mashambulio zaidi yakishuhudiwa katika eneo hilo wakazi wamekimbia maeneo ya Kaben na Sambalat karibu na mpaka wa Pokot Magharibi.

2 Comments

  1. Napoleon January 29, 2022

Leave a Reply