Shabiki Mkongwe wa Harambee Stars na AFC Leopards Isaac Juma,58, ameaga dunia kufuatia shambulio la mshambuliaji nyumbani kwake kijijini Ebuyenjeri, Mumias, Kaunti ya Kakamega.

Maafisa wanaoshughulikia suala hilo walisema uchunguzi wa awali ulihusisha mauaji yake na mzozo wa ardhi katika eneo hilo kitu ambacho pia DCI wamethibitisha.
Maafisa walisema Juma aliuawa kwa kukatwakatwa na mshambulizi mnamo Jumatano mwendo wa saa tano usiku.
Juma alikuwa mpenzi wa soka na aliunga mkono kwa dhati timu ya taifa, Harambee Stars na ile ya AFC Leopards.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi kanda ya Magharibi Peris Muthoni, mtuhumiwa wa mauaji ya Juma amekamatwa na anazuiliwa katika kituo cha polisi wakiendelea kumhoji mshukiwa kwa habari zaidi vilevile akisubiri kufikishwa mahakamani siku ya Ijumaa ya tarehe 28 Januari kwa kesi ya mauaji.
.
“Tuna mshukiwa wa mauaji hayo kujua zaidi,” alisema.
Mtuhumiwa huyo kwa kwa jina Milton Namatsi, 27, amekamatwa nyumbani kwake Mumias na makachero wa kitengo cha DCI baada ya uchunguzi wa awali kuonesha kuwa Namatsi alikuwa na ushawishi mkubwa katika mauaji ya shabiki huyo wa spoti.
Mkewe kwa jina Farida akizungumza na kituo kimoja cha habari nchini Kenya amesema kuwa kisa hicho kilitokea kutokana na mzozo wa ardhi ambao umekuwa ukiendelea.
“Aliniambia alikuwa na masuala ya ardhi katika eneo hilo, na ikitokea kifo chake, niwaambie mamlaka kwamba ni kwa sababu ya mgogoro wa ardhi.” mkewe Juma amesema.
Marehemu ambaye anatajwa kuwa mchuuzi wa magazeti jijini Nakuru kabla ya kustaafu na kurudi nyumbani kwake Mumias alikuwa ni shabiki wa kufa kupona wa michezo nchini Kenya huku akitajwa kuwa mshupavu huyo namba moja wa timu ya taifa Harambee Stars na AFC Leopards.
Mwili wake Juma ulichukuliwa baadaye na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti huku uchunguzi ukiendelea.
Hata hivyo, Watu mbalimbali wametuma jumbe za rambirambi kwa familia ya mwendazake Juma huku wakionyesha mshtuko mkubwa kutokana na kifo cha ghafla cha Isaac Juma.
Hizi ni baadhi ya jumbe za waliomuomboleza Juma.
Naibu Rais William Ruto, “Tumehuzunishwa na kumpoteza shabiki wa muda mrefu wa AFC Leopards na Harambee Stars Isaac Juma. Alikuwa mfuasi wa soka wa kirafiki, mcheshi na mwenye shauku.” Mawazo yetu yapo kwa familia na wapenda soka katika kipindi hiki kigumu. lala salama Juma.”
Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, “Juma alikuwa mpenda soka aliyejitolea na kujiburudisha ambaye alivutia shughuli nyingi za michezo katika kaunti na nchi nzima,” alisema.
Chama cha kisiasa cha odm, kikiongoza na kinara wao Raila Odinga pia waliomboleza kifo cha shabiki huyo;
“Tunaomboleza mauaji ya Bw. Isaac Juma Onyango, shabiki mashuhuri wa kandanda na mfuasi mkubwa wa kiongozi wa chama chetu. @RailaOdinga Jumanne usiku nyumbani kwake Mumias. Tunavitaka vyombo husika vya ulinzi na usalama viende kwa kasi kuwafikisha wauaji wake kwenye hati fungani.”