Msemaji wa Serikali ya Somali ajeruhiwa katika shambulio la kigaidi.

Mohamed Ibrahim Moalimuu, mwandishi wa habari wa zamani wa BBC, ambaye pia ni msemaji wa Serikali ya Somalia,amejeruhiwa katika shambulio baya la kigaidi kwenye gari lake siku ya leo,Jumapili.

Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble amesema kuwa Shambulio hilo baya la kigaidi  limetokea kwenye makutano ya barabara katika mji mkuu,Mogadishu ambapo Bwana Moalimuu amejeruhiwa na kukimbizwa hospitalini  baada ya mlipuko wa bomu kutokea na hali yake inaendelea vizuri.

Shambulio hili linakuja siku chache baada ya lingine lililoua takriban watu wanane – lile lililotekelezwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabab karibu na kambi ya Jeshi la Wana-anga la Somalia na uwanja wa ndege wa kimataifa.

Kundi la Al-Shabab limekuwa likipambana na serikali ya Somalia kwa zaidi ya muongo mmoja, na linashikilia ngome katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Mashambulio haya ya hivi karibuni yanatokea huku kukiwa na mvutano wa kisiasa wa miezi kadhaa kati ya waziri mkuu na rais kuhusu uendeshaji wa uchaguzi uliocheleweshwa.

Hata hivyo shambulio hili linakuja siku chache tu baada ya

makubaliano kati ya viongozi wa majimbo na waziri mkuu wa Somalia ya kuharakisha uchaguzi ndani ya siku 40 – kuanzia tarehe 15 Januari 2022 na kukamilika Februari 25.

Kundi la wanamgambo wa kiislamu la al-Shabab  lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda limekuwa likiendesha kampeni kali ya mashambulizi dhidi ya serikali kuu dhaifu tangu 2007,limedai kuhusika na Shambulio hilo la leo Jumapili 16.

Leave a Reply